Makamu wa Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua ameshtushwa na uamuzi wa Mahakama Kuu nchini humo kuruhusu Shirika lisilo la kiserikali (NGO) linaoundwa na watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja lisajiliwe.

Mahakama Kuu ilitoa uamuzi katika shauri lililofunguliwa na kundi la watu waliokuwa wanapinga uamuzi wa Serikali kukataa kusajili NGO ya watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja. Kwa mujibu wa Mahakama, uamuzi wa Serikali ulikuwa wa kibaguzi.

Makamu wa Rais alisema kuwa alishtushwa na uamuzi huo wa Mahakama kiasi cha kushindwa kuongea kuhusu jambo hilo.

“Mimi nilishangaa nikashindwa kuongea, unajua unaweza shangaa ushindwe kuongea… Yale maneno tunasikia pale kotini, eti kuna chama ya kutetea eti wanaume waoe wanaume, na wanawake waoe wanawake… sasa hiyo ni mambo gani hiyo?” Alihoji.

Makamu wa Rais alisisitiza kuwa hawatakubali mambo ya ushoga kwakuwa wao ni wacha Mungu na mambo hayo ni ya kishetani.

“Kiongozi wa hii nchi ni mcha Mungu na tutafanya kile ambacho anataka tufanye, tuna mila na desturi zetu na mambo wanayotaka tukubaliane nayo ni kinyume cha maadili, haki na mfumo wetu wa maisha,” Gachagua aliongeza.

Uamuzi huo pia uliamsha hasira kwa baadhi ya wanasiasa ambao walipendekeza kuwa Mahakama iangaliwe kwakuwa imepata msukumo kutoka nchi za Magharibi. Hata hivyo, wapo wanaotetea uamuzi wa Mahakama wakisema kundi hilo la watu lilikuwa na nia ya kutetea haki za binadamu.

Wabunge wa Kenya pia wanataka Mahakama Kuu iangaliwe kwa kujaribu kuhalalisha mambo ya ushoga kwa lengo la kuyaridhisha mataifa ya Magharibi.

Mbunge wa Homa Bay, Peter Kaluma yeye alisema kuwa watarejea mahakamani kuomba uamuzi huo upitiwe upya kwani kuna baadhi ya majaji kati ya saba hawakuwepo.

“Nitachukua uamuzi, kwakuwa kati ya majaji watatu wa Mahakama Kuu waliamua kuwa NGO hiyo isajiliwe, wawili walikataa na wawili hawakuwepo, tutarejea mahakamani hapo wakati majaji wote saba watakaa na kufanya mapitio,” alisema Kaluma.

Fidia kwa Wafanyakazi: WCF yaboresha huduma kimtandao
Bilioni 313 zawanufaisha Wajasiriamali sekta ya Kilimo