Mgombea urais wa Kenya, Mukhisa Kituyi ametangaza kujitoa kwenye kinyang’anyiro cha urais na kumuunga mkono Raila Odinga.
Kituyi ambaye ni Katibu Mkuu wa zamani wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalojishughulisha na maendeleo ya biashara (UNCTAD), amesema amechukua uamuzi huo baada ya kufanya mazungumzo na Odinga.
Aidha, Kituyi alitupa kombora kwa Makamu wa Rais, William Ruto ambaye anagombea pia urais, akisema kuwa moja ya malengo yake ya kujiengua kwenye kinyang’anyiro hicho cha urais ni kuhakikisha mtu fulani hapati nafasi ya kurithi kiti alichokalia Rais Uhuru Kenyatta.
“Ni muhimu sana kuhakikisha kwamba mtu fulani anazuiwa kwa nguvu zote kuusogelea urais wa Kenya milele,” alisema.
Hata hivyo, Kituyi alisema kuwa hajaiacha ndoto yake ya kuwania urais, lakini sasa hivi ameweka kipaumbele katika kuhakikisha Odinga anaibuka mshindi.
Odinga ambaye anaungwa mkono na Rais Kenyatta anachuana vikali na Ruto kwenye uchaguzi huu.
Baadhi ya wachambuzi wanatabiri kuwa huwenda kukawa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya uchaguzi.