Mzozo kati ya makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), umeongezeka zaidi baada ya pande hizo mbili kila moja kuteua mawakili tofauti wa kuwawakilisha katika ombi la kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais wa Agosti 9, 2022.
Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa IEBC, Hussein Marjan aliifahamisha Mahakama ya Juu kuwa wameteua mawakili 26 watakaoiwakilisha tume hiyo na mwenyekiti wake Wafula Chebukati, uamuzi ambao utamuathiri mlipa kodi wa Taifa la Kenya kutokana na gharama ambazo zitatumika.
Uteuzi huo, uliowasilishwa na Marjan haukuwa na uwakilishi wa makamishna wengine sita, akiwemo Prof. Abdi Guliye na Boya Molu, waliorodheshwa kama wajibu wa maombi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais wa Agosti 9.
Hata hivyo, baadhi ya makamishna walionekana kutofahamu kuhusu uteuzi wa mawakili hao, ambapo awali Makamu mwenyekiti wa IEBC, Juliana Cherera na makamishna Francis Wanderi, Justus Nyang’aya na Irene Masit walikataa matokeo yaliyotangazwa na Chebukati.
Kati ya kampuni 26 za mawakili zilizopewa kandarasi na tume hiyo, 22 zitawakilisha IEBC ambayo ni mlalamikiwa wa kwanza huku nne zikichukua nafasi ya Chebukati ambaye ni mtu wa kwanza wa kuwajibika na kesi hiyo tuhumiwa kutokana na kusimamia zoezi zima la uchaguzi wa urais.
Mawakili hao, watakuwa wakitetea uendeshaji wa uchaguzi pekee bali pia masuala ya Chebukati ambaye anakabiliwa na shutuma nyingi na baadhi ya makosa ya jinai.