Kiongozi wa azimio La Umoja One nchini Kenya, Raila Odinga amezungumza hadharani kwa mara ya kwanza tangu Mahakama ya Juu kuidhinisha matokeo ya uchaguzi wa urais na kukashifu uamuzi huo huku akisema wataendelea kuongea kwa kuwa ni haki yao.
Odinga, ameyasema hayo Septemba 15, 2022 wakati akiongea huku akiwa na hasira mjini katika Hotel ya Sarova Whitesand iliyopo mjini Mombasa na kusema familia ya Azimio ilishangazwa na uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Juu, huku akiinenea mema Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC.
Amesema, “Inasikitisha watu wa nchi hii walipiga kura lakini Jose Camargo wa Venezuela anakuja kuamuru nani atakuwa Rais wa nchi hii, sisi tuliheshimu mahakama kuu lakini hatukubaliani na matokeo na tunasubiri hukumu ya mwisho waliyosema watatoa kwa sababu tumesalia na chini ya siku 10.”
Odinga amefafanua kuwa, “Mashine iliyotumika kusambaza matokeo Meru ni ile ile iliyotumika Nyeri na wanaamua kulichukulia suala hilo kirahisi ni aibu kwa Mahakama na ninaona wanajaribu kutishia watu lakini tutazungumza kwa sababu ni haki yetu.”
Aidha ameongeza kuwa, “Hatutaruhusu Idara ya Mahakama kuwa dikteta, tutalinda haki za watu wa Kenya jinsi inavyohitajika katika Katiba kwanini watu wa nchi hii waamke mapema kupiga kura na kupoteza muda wao? IEBC ni taasisi nyingine mbovu.”
Hata hivyo, Raila Odinga, amemaliza kwa kusema, “Bado sikuwa tayari kutoa hotuba ya umma lakini hii ni moja ya hafla ambazo ninahitaji kutoa taarifa nilikuwa nje ya nchi (Zanzibar) na familia yangu na kwa hivyo sikufika kwenye sherehe ya kuapishwa lakini nina furaha kuwa hapa.”