Kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga amesisitiza kuwa ataheshimu uamuzi wa mahakama ya Juu, baada ya yeye na mgombea mwenza wake Martha Karua, kuwasilisha ombi katika Mahakama kuu ya nchi hiyo Agosti 22 kupinga matokeo ya uchaguzi wa Agosti 9, 2022 .
Katika kikao na Wanahabari, Odinga alithibitisha imani yake kwa uamuzi utakaotolewa na Mahakama ya Juu, licha ya kudai kuwa alishinda uchaguzi wa urais uliofanyika nchini Kenya na kuilaumu tume Huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC).
Amesema ana uthibitisho kwamba alishinda uchaguzi huo, unaohitaji mgombea kupata asilimia 50 ya kura pamoja na moja, na kwamba kuna mambo hayakuwa sawa ikiwemo utaratibu wa utangazaji wa matokeo na mgawanyiko wa makamishna wa IEBC.
Tangu 2002, hakuna uchaguzi wa urais nchini Kenya ambao haujapingwa, na matokeo ya mwaka huu pia yamesababisha mpasuko ndani ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), ambayo ilisimamia uchaguzi huo.
Kulingana na nakala ya ombi hilo la kurasa 72 la timu ya Odinga inadai kuwa mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati alishindwa kujumlisha takriban kura 140,000 ambazo zingeweza kubadili matokeo.
Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 77, alipoteza nia yake ya tano ya kugombea urais kwa tofauti ndogo ya takriban kura 230,000, chini ya asilimia mbili ya pointi, huku majaji wakiwa na chini ya wiki moja kutoa uamuzi na iwapo watabatilisha matokeo ya IEBC, kura zitapigwa tena ndani ya siku 60.