Kiongozi wa Azimio la Umoja na aliyekuwa mgombea urais wa Muungano wa Kenya, Raila Odinga amesema chama hicho kitapinga tamko la IEBC, kumtangaza William Ruto kuwa rais mteule hapo kesho Agosti 22, 2022.
Akizungumza katika ibada ya Kanisa la Jesus Teaching Ministry (JTM), la Donholm jijini Nairobi hii leo Agosti 21, 2022, Odinga ambaye aliandamana na mgombea mwenza Martha Karua na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka walisema hawawezi kuruhusu sauti za Wakenya zifutwe.
“Hakuna shaka katika akili zetu kwamba watu wa Kenya walizungumza kwa sauti kubwa tarehe 9 Agosti, lakini sauti yao haitazimwa na ushindi wao hautapokonywa,” amesema Odinga.
Kwa upande wake mgombea mwenza wa Odinga, Bi. Martha Karua amesema kambi yao hatimaye itapata haki kutoka kwa Mahakama ya Juu na kudai kuwa “Tutajua ukweli na utatuweka huru sote kwani bila haki hakuwezi kuwa na amani ya kudumu.”
Naye mratibuwa uchaguzi wa Odinga, Kalonzo Musyoka amebainisha kwamba wana uhakika wa kuibuka washindi katika Mahakama ya Juu na kuwataka Wakenya kusimama kwa pamoja kwa utulivu ili waone wokovu wa Mungu.
“Tunaondoka mahali hapa tayari kuwafuata na jukumu la kuwafuata limewasilishwa ipasavyo hivyo ninawaomba Wakenya tafadhali simameni tuli muone wokovu wa Mungu.” amesema Musyoka.
Alisema uchaguzi wa Agosti 9 bado haujakamilika kutokana na uchaguzi unaokaribia Mombasa, Kakamega na vitengo vingine vinne vya bunge na kwamba, “Mimi ninavyofahamu, Mwanasheria aliye ndani yangu ananiambia Uchaguzi Mkuu huu haujaisha.”
Aidha, Musyoka amebainisha kuwa, kinachoendelea katika miji ya Mombasa, Kakamega na maeneo mengine ya ubunge ni kisa cha wazi ambacho kinaonesha Wakenya wamebadilishwa kwa muda mfupi.