Rais wa Kenya, William Ruto amekutana na Viongozi wa Kenya Kwanza ili kuelezea ajenda yake ya kisheria, mpango wa kukabiliana na gharama za juu za maisha zilizozidishwa na kupanda kwa bei ya mafuta na umeme, na kuhimiza uidhinishaji wa haraka wa wateule wa Baraza la Mawaziri.
Katika mkutano huo wa siku mbili, ulioanza Septemba 15, na unaotarajia kufikia tamati hii leo Septemba 16, 2022, Ruto atatumia fursa hiyo kutengeneza timu itakayoharakisha ajenda yake katika Seneti na Bunge la Kitaifa, huku ajenda zake nyingi zikihitaji uzingatiaji wa sheria.
Aidha, Rais Ruto pia anatazamia kuona kamati kuu za Bunge zikidhibitiwa na wabunge kutoka kambi yake isipokuwa Kamati ya Uhasibu wa Umma, Kamati ya Uwekezaji wa Umma na Kamati ya Utekelezaji, ambazo zimetengwa kwa muungano ambao haujaunda Serikali.
Ili kukabiliana na changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira kwa vijana, Ruto amesema utawala wake utaanzisha mpango wa makazi ya kijamii na wa bei nafuu, unaolenga wastani wa vitengo 250,000 kwa mwaka, huku akitazamia pia kuweka ushawishi kwa kambi ya Odinga ili kumpa udhibiti wa Mabunge yote mawili.
Kikao hicho, pia kitajadili kuidhinishwa kwa wajumbe wa Baraza la Mawaziri na jinsi wabunge watakavyotakiwa kuongeza kasi ya uhakiki wao ili kumruhusu Rais kutekeleza ajenda yake ya kuinua uchumi wa nchi ulikumbwa na msukosuko wa vita vya Ukraine na uwepo wa Ugonjwa wa Uviko-19.
Ajenda nyingine itakayojadiliwa, ni kupunguza bei ya mafuta iliyopanda baada ya kusimamisha ruzuku, huku Msajili wa Vyama vya Siasa, Anne Nderitu akisema licha ya muungano wa Azimio kuwa idadi kubwa ya viti vya Bunge la Kitaifa, bado hautatoa kiongozi kutokana na kasoro zilizojitokeza baada ya uchaguzi.