Serikali ya Kenya imetangaza marufuku ya uchinjwaji wa punda nchini humo ili kuzuia kutokomea kwa wanyama hao ambao idadi yao inasemekana kupungua.
Waziri wa kilimo peter Munya alitangaza kufungwa kwa machinjio yote ya punda baada ya wakulima kuandamana nje ya ofisi yake wakidai kutoweka kwa punda ambao huwasaidia kubeba mizigo.
Kwa mujibu wa ripoti ya shirika linalotetea maisha ya wanyama -Africa network for Animal Welfare punda nchini kenya wanakabiliwa na uwezekano wa kutoweka ifikapo mwaka 2030 ikiwa hawatalindwa.
”Sasa hivi bei ya punda imefikia kati ya shilingi 15,000 , elfu 20,000 kwasababu punda wamechinjwa, wameliwa na wachina”, alisema mmoja wa wakulima wenye hasira katika mahojiano na kituo kimoja cha habari nchini Kenya”.
Waziri Peter Munya alisema: ”Tunawapatia kipindi cha mwezi mmoja wamiliki wa machinjio ya punda kubadili machinjio na kuwa machinjio ya wanyama wengine wa kawaida.
Tangazo la marufuku ya machinjio ya punda limekua ni ahueni kwa wakulima na wanaharakati wa haki za wanyama ambao kwa muda wamekua wakipinga kuchinjwa kwa nyama ya punda nchini Kenya.
Kwa miaka kadhaa wamekua wakiandamana katika maeneo ya Baringo, Machakosi na Turkana wakidai kuongezeka kwa uhitaji wa nyama ya punda kumesababisha kuongezeka kwa wizi wa punda.