Waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Ulaya wamesema uchaguzi nchini Kenya ulikuwa na mvutano mdogo ikilinganishwa na chaguzi zilizopita.
Waangalizi hao, hata hivyo waliibua wasiwasi kuhusu mchakato wa kuhesabu kura kwa kile walichodai kuwa wametengwa.
Wamesema mchakato huo wa kuhesabu na kujumlisha kura ambao unaendelea nchini Kenya unatarajiwa kuchukua siku na hivyo kuongeza wasiwasi baina ya wapiga kura.
Kulingana na ujumbe wa EU, kipengele kingine ambacho hakijashughulikiwa ipasavyo katika uchaguzi huo ni pamoja na ukosefu wa mfumo wa fedha wakati wa kampeni.
Hata hivyo, matokeo ya muda yanayoendelea kutolewa bado yanaonesha ushindani mkali katika nafasi ya urais.
Waangalizi hao wa kimataifa pia wanasema upo uwezekano wa kuenea kwa kasi kwa taarifa potofu, kupitia mitandao ya kijamii ambayo nayo inaharakisha utoaji wa matokeo.