Wakati Wakenya wakiendelea kupiga kura katika vituo mbalimbali kuchagua viongozi wao wa ngazi tofauti, hitilafu zimeendelea kuonekana katika baadhi ya maeneo.

Eneo la Rongai kaunti ya Nakuru Uchaguzi wa kiti cha ubunge umeahirishwa baada ya hitilafu kwenye karatasi za kupigia kura ambapo tangazo hilo limetolewa Jumanne Agosti 9 wakati wa kupiga kura baada ya kubainika kuwa kuna mchanganyiko wa karatasi za kura.

Inasemekana kwamba karatasi hizo zimechanganyika na za Kuresoi Kusini katika kaunti hiyo ya Nakuru lakini umbali mrefu.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati pia Jumatatu Agosti 8 alisitisha uchaguzi wa ugavana Kakamega na Mombasa kwa sababu ya mchanganyiko wa picha za wagombea.

Akizungumza wakati wa kikao na wanahabari katika eneo la Boma Kenya, Chebukati alieleza kuwa uamuzi huo ulifikiwa baada ya tume hiyo kubaini kuwa karatasi za kupigia kura zilikuwa na maelezo yasiyo sahihi ya wagombeaji.

Afisa wa Usimizi wa Kura akizungumza na wapiti kura. Picha:Tuko News

Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya ameibua maswali kuhusu uamuzi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) wa kusitisha uchaguzi wa ugavana katika kaunti za Kakamega na Mombasa akihoji sababu za zoezi hilo kuahirishwa katika kaunti anazotaja kuwa ngome za mgombea wa urais wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya.

“Uamuzi wa IEBC kuahirisha uchaguzi wa ugavana katika kaunti za Kakamega na Mombasa ni njama ya kuiba uchaguzi. Ninashindwa mbona waliamua kusitisha chaguzi za ugavana katika ngome za mgombea wa Azimio Raila Odinga na nyumbani kwa viongozi wawili wakuu wa chama cha ODM,” alisema.

“Ninaogopa kuwa hatua hiyo itaathiri idadi ya wapiga kura watakaojitokeza katika kaunti hizo mbili ambazo Raila alikuwa anategemea kwa idadi kubwa ya kura kumpa ushindi. Tangazo hili limesababisha taharuki katika kaunti na linaweza kuzua vurugu iwapo halitashughulikuwa ipasavyo,” Oparanya aliongeza.

Mgombea wa ugavana Mombasa kwa tiketi ya UDA Hassan Omar alisema ilikuwa pigo kubwa kusitisha uchaguzi huo.

“Ni jambo la kuudhi sana ikizingatiwa kuwa tumefanya kazi kubwa sana. Na tunajiuliza maswali ni vipi IEBC ilifanya kosa hilo,” alisema Omar.

Katika kaunti ya Kirinyaga, kura za ugavana zilipatikana katika eneo la Mumias Mashariki ambapo Gavana Ann Waiguru anayewania kiti hicho tena na tiketi ya UDA alishangaa ni vipi kura hizo zilifika huko.

Kwa mujibu wa takwimu za IEBC, wapiga kura 22,120,458 waliosajiliwa watapiga kura mwaka huu kuwachagua Wabunge 290 wa Bunge la Kitaifa, madiwani 1,450, maseneta 47, magavana na wawakilishi wanawake, pamoja na mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta.

Kocha Bakari Shime kicheko Serengeti Girls
Kenya: Martha Karua abadilishiwa kituo cha upigaji kura