Rais mteule wa Kenya, William Ruto, ameitaka mahakama ya juu ya nchini humo kutupilia mbali kesi iliyowasilishwa na Raila kwa sababu anataka mgao wa serikali.
Kauli hiyo ya Ruto ipo katika kurasa 256 za majibu aliyowasilisha kwa kile alichopinga Raila Odinga wa Azimio kuhusu ushindi wake kwenye uchaguzi wa Agosti 9.
Ruto ameongeza kwamba Raila ana rekodi za kupinga kila matokeo ya uchaguzi mkuu, kiasi cha kulazimisha maelewano yatakayomwezesha kupata sehemu ya serikali.
Kenya: Malema amuita Odinga wamuunge mkono Ruto
Katika Mahakama ya Juu Ruto alitoa mfano wa serikali ya nusu mkate iliyoundwa baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2007, enzi za Mwai Kibaki na mwaka 2017 waliposalimiana na Rais anayeondoka Uhuru Kenyatta.
Kikosi cha wanasheria wa William Ruto kimesema kuwa kina uhakika wa kuwa Mahakama itatupilia mbali upingaji huo wa matokeo na Ruto ataapishwa kama rais wa Kenya.
Wakili Kithure Kindiki akizungumza wakati akiwasilisha majibu ya madai ya udanganyifu alisisitiza kuwa Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua walichaguliwa kihalali.
“Tumejipanga sisi. Tunatazamia kudhihirisha kwamba William Ruto na Rigathi Gachagua walichaguliwa kihalali kama ilivyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) mnamo Jumatatu, Agosti 15,” Kindiki alisema.
Ruto alipuuzilia mbali madai ya mgombea urais wa Azimio la Umoja One Kenya Coalition, Raila Odinga kwamba fomu 34A na 34B zilibadilishwa kwa ajili ya kumpa ushindi.
Kiongozi huyo wa Muungano wa Kenya Kwanza alisema fomu hizo zilitayarishwa mbele yake na kutiwa saini na mawakala wa wagombeaji.
“Mashahidi wangu Raymond Kiprotich Bett na Koech Geoffrey Kipngosos wamenishauri kwamba haiwezekani kwa vyovyote vile kutayarisha, kubadilisha na kutupa zaidi ya fomu 11,000 za 34A ndani ya dakika nane kama ilivyodaiwa katika ombi, au hata kidogo,” Ruto alisema.
Katika mkakati wa Ruto, kikosi cha mawakili 54 kinajiandaa kuhakikisha kuwa Mahakama ya Upeo imeidhinisha kuchaguliwa kwa William Ruto kama rais wa tano wa Kenya.
Hata hivyo, Kenya Kwanza na kikosi chao cha mawakili kinaongozwa na Fred Ngatia ambaye anajulikana kwa kuwa mahakamani.