Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amepinga kufanyika kwa mazungumzo yoyote na kiongozi wa upinzani Raila Odinga kumaliza mgogoro wa kisiasa nchini humo uliosababishwa na uchaguzi mkuu uliokwisha.

Akitoa hotuba muda mfupi baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa marudio , rais Kenyatta amesema kuwa mpinzani wake Raila Odinga atakwenda mahakamani kwa mara nyengine tena kupinga uchaguzi wake.

Kenyatta amewataka wapinzani wake wa NASA kutumia njia zote za kisheria katika kupigania haki yao kwani hakuna mtu yeyote atakayewadhulumu haki yao ya kikatiba.

Katika uchaguzi wa marudio Uhuru alijipatia kura 7,483,895 huku Raila Odinga akijipatia kura 73,228 hata baada ya kujiondoa katika uchaguzi huo huku rais Kenyatta pia akimshutumu Raila Odinga kwa kujiondoa katika uchaguzi huo.

”Licha ya kwamba mpinzani wangu mkuu alienda mahakamani akitaka uchaguzi wa urais kufutiliwa mbali na akakubaliwa, aliamua kutotilia maanani uamuzi wote kwa pamoja ambao uliagiza kufanyika kwa uchaguzi katika kipindi cha siku 60 uliosimamiwa na IEBC. Baadaye alikaataa kushiriki katika uchaguzi,” amesema Kenyatta.

 

Moses Basena aomba kupandishwa cheo Uganda
TFF yashtukia njama za kumchafua Rais Karia