Klabu ya Chelsea imethibitisha kukamilisha usajili wa mlinda mlango kutoka nchini Hispania Kepa Arrizabalaga, kwa ada ya Pauni milioni 71.6 akitokea Athletic Bilbao.
Kepa mwenye umri wa miaka 23, anajiunga na wababe hao wa magharibi mwa jijini London, na kuweka rekodi ya kuwa mlinda mlango aliyesajiliwa kwa gharama kubwa duniani, akivunja rekodi iliyowekwa majuma mawili yaliyopita na mlinda mlango kutoka nchini Brazil Alisson Becker, wakati akisajiliwa na majogooo wa jiji Liverpool akitokea AS Roma ya Italia kwa ada ya Pauni milioni 66.9.
Usajili wa Kepa ulikamilishwa usiku wa kuamkia hii leo, baada ya viongozi wa pande zote mbili kufikia makubaliano, ikiwa ni saa 48 baada ya kukutana na kuanza mazungumzo ya uhamisho wa mlinda mlango huyo ambaye anakwenda kuanza maisha mapya nchini England.
Usajili wa mlinda mlango huyo una kusudio la kuziba nafasi ya Thibaut Courtois ambaye usiku wa kuamkia jana alikamilisha mpango wa kujiuunga na mabingwa wa soka barani Ulaya/Duniani, Real Madrid.
Alisson Becker
Akizungumza mara baada ya kukamilisha taratibu za usajili wake huko Stamford Bridge Kepa alisema: “Nimefanya maamuzi sahihi ya kuja hapa, ninaamini soka langu litaendelea kukua na kupata changamoto tofauti na nchini Hispania, Chelsea ni klabu yenye lengo la kusaka mafanikio katika ligi ya ndani na nje ya mipaka ya England.
“Kuna mambo mengi yaliyonivutia hadi kufikia hatua ya kukubali kuja hapa, ninaifahamu vizuri klabu hii, nimekua mfuatiliaji mzuri wa michezo yake tangu nikiwa Hispania, ninafurahi sana kuwa sehemu ya kikosi cha Chelsea, ninaamini nitasaidia na kuwa sehemu ya mafanikio yatakayopatikana kuanzia msimu wa 2018/19.”
Kepa anakua mchezaji wanne kusajiliwa na klabu ya Chelesea katika kipindi hiki cha usajili wa majira ya kiangazi, akitanguliwa na Jorginho kutoka SSC Napoli, Robert Green (Mchezaji huru) pamoja na Mateo Kovacic akitokea Real kwa mkopo.
Kepa anaondoka nchini Hispania baada ya kucheza michezo 53 ya ligi ya nchi hiyo (La Liga), kwa misimu miwili akiwa na klabu ya Athletic Bilbao.
Anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha Chelsea kitakachoanza katika mchezo wa kwanza wa msimu wa ligi ya England mwishoni mwa juma hili dhidi ya Huddersfield Town.