Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa ameitaka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira – RUWASA, kuunganisha mabomba ya Maji yanayotajwa kuwepo kwa muda mrefu katika maeneo ya Kata ya Igoma iliyopo Halmashauri
ya Wilaya ya Mbeya na kupelekea Wakazi wa maeneo hayo kulalamikia uwepo wa kero ya maji.
RUWASA imepewa agizo hilo mara baada ya Wakazi wa Igoma kuiomba Serikali kusaidia kutatua kero ya Maji iliyodumu kwa miaka mingi, licha ya kuwepo kwa mabomba hayo, ambapo DC Malisa na alimuagiza Meneja wa RUWASA kulishughulikia suala hilo ndani ya wiki mbili, kwa
kuanza kuyaunganisha mabomba hayo.
Kwa upande wake Meneja wa RUWASA, alisema tayari Serikali imetoa fedha kwa ajili ya kuanza kusambazwa na kuunganishwa kwa mabomba hayo ya maji haraka na ndani ya wiki mbili Wakazi wa Igoma wataanza kuwa na matumaini ya kupata huduma muhimu ya maji.
Hata hivyo, Malisa amewahidi wakazi wa kata hiyo kufuatilia kwa umakini maelekezo aliyoyatoa na ikiwezekana ndani ya wiki mbili za maelekezo atatembelea Igoma kuona hatua zilizochukuliwa.