Jumuiya ya Wafanyabishara nchini imekutana na Wafanyabishara wa Mkoa wa Tanga ili kusikiliza kero na kuchukua maoni mbalimbali kwa ajili ya kuyapeleka Serikalini, ikiwa ni agizo la Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa alilolitoa hivi karibuni, ili kuweza kuyafanyia kazi ikiwa ni lengo la Serikali kuweka mazingira rafiki katika sekta ya Uchumi.
Akizungumza mara baada ya mkutano huo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabishara nchini, Hamis Livembe amesema pamoja na kuzunguka kila Mkoa kukusanya maoni hayo, pia wana lengo la kusajili wanachama wapya katika jumuiya hiyo.
Amesema, “sasa hivi wafanyabishara wana hamu kubwa baada ya lile sakata kubwa la kufungwa maduka kule Kariakoo Dar es salaam imeundwa kamati baada ya kurudi huko wanataka watusikie kuna nini kipya lakini pia tunatoa mrejesho kwa yale ambayo tayari tumeshapata majibu.”
Kwa upande wake, Katibu wa Jumuia ya Wafanyabishara wa Mkoa wa Tanga, Masoud Ismaili amesema bado zipo changamoto lukuki zinazo wakabiri Wafanyabishara, ikiwemo kupandishiwa makadirio ya kodi sambamba na usumbufu wa ushuru kutoka jambo ambalo linawakatisha tamaa ya ulipaji kodi kwa hiari.