Kesi ya kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo na kutakatishaji fedha, inayomkabili rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na makamu wake Geofrey Nyange ‘Kaburu’, imeahirishwa baada ya upande wa mashtaka kudai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.
Aveva na Nyange wanakabiliwa na mashtaka matano likiwemo la kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha fedha USD 300,000, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Hata hivyo, mshtakiwa kwanza katika kesi hiyo, Aveva ameruhusiwa kutoka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa akitibiwa maradhi ya figo, lakini ameshindwa kufikishwa mahakamani hapo kutokana na hali yake kutotengemaa vizuri
Wakili wa Takukuru, Leonard Swai, alidai hayo leo katika Mahakama ya Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Victoria Nongwa wakati shauri hilo lilipofikishwa kwa ajili ya kutajwa.
“Tumepata taarifa kuwa mshtakiwa anaendelea vizuri na ameshatoka hospitali, yupo gerezani leo hajaletwa mahakamani hapa kwa sababu bado afya yake haijatengemaa vizuri, hiyo tutakwenda kuchukua maelezo yake kama tulivyochukua ya mshtakiwa wa pili, kwa sababu hapo awali tulishindwa kumchukua maelezo yake kwa sababu alikuwa mgonjwa na isingekuwa busara kumhoji mshtakiwa ambaye ni mgonjwa, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa” alidai Swai.
Baada ya maelezo hayo hakimu, Nongwa aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 22, mwaka huu itakapotajwa.
Katika shtaka la kwanza, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa walikula njama ya kughushi fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15,2016 wakionesha Klabu ya Simba inalipa mkopo wa USD 300,000 kwa Evans Aveva wakati si kweli.
Katika shtaka la pili alidai kuwa Machi 15,2016 katika benki ya CRDB tawi la Azikiwe Ilala Aveva akijua alitoa nyaraka za uongo ambayo ni fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15,2016 wakati akijua ni kosa.
Ilidaiwa katika shtaka la tatu la kutakatisha fedha, Aveva na Nyange wanadaiwa kuwa kati ya Machi 15 na Juni 29,2016 Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama ya kutakatisha fedha kwa kupata mkopo wa USD 300,000 wakati wakijua ni zao la uhalifu.
Kwa upande wa shtaka la nne la kutakatisha fedha, Aveva anadaiwa kuwa kati ya Machi 15,2016 katika benki ya Baclays Mikocheni alijipatia USD 300,000 wakati akijua zimetokana na kughushi.
Katika shtaka la tano la kutakatisha fedha, mshtakiwa Nyange anadaiwa kuwa Machi 15,2016 katika benki ya Baclays tawi la Mikocheni alimsaidia Aveva kujipatia USD 300,000 wakati akijua fedha hizo zimetokana na kughushi.