Kesi inayowakabili viongozi wa juu wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na Geofrey Nyange ‘Kaburu’ imeahrishwa kwa mara nyingi tena hadi Aprili 12, 2018 kufuatia ombi la upande wa mashtaka kudai wanataka kumuongeza mshtakiwa mmoja katika kesi hiyo.
Hayo yamesemwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu Jijini Dar es Salaam, Thomas Simba, na Wakili wa Serikali kutoka TAKUKURU, Leornad Swai, ambapo amesema kuwa kesi hiyo ilifikishwa Mahakamani hapo kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali baada ya upelelezi wa kesi yao kukamilika.
Wakili Swai aliiomba Mahakama ahirisho fupi kwa kuwa wanatarajia kufanyia mabadiliko katika hati ya mashtaka kwa kuongeza mshtakiwa mmoja.
Aidha, Kufuatia ombi hilo, Mahakama iliamua kuahirisha kesi hiyo hadi Aprili 12 mwaka 2018 kwa ajili ya upande wa mashtaka kufanya mabadiliko yao na washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.
Hata hivyo, Aveva na Kaburu kwa pamoja walipandishwa Mahakamani kwa mara ya kwanza Juni 27 mwaka 2017 wakiwa wana kabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi ikiwemo ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na utakatishaji wa fedha.