Kesi iliyofunguliwa Mkoani Mbeya, ya kupinga mkataba baina ya Serikali ya Tanzania na Falme ya Dubai wa ushirikiano wa uendelezaji wa Bandari haina zuio, hivyo mchakato wake unaweza kuendelea kwa jinsi watakavyoona na kama pande mbili zitakaa tena kuongeza muda wa majadiliano.
Hayo yamebainishwa hii leo Julai 28, 2023 na Mbunge wa Ukonga Jerry Silaa na kuongeza kuwa Watanzania wote wana haki ya kuzungumzia mkataba huo, lakini lazima uwekwe kisheria kwani kuna wapotoshaji wasiotumia hoja za msingi.
“Kesi iliyofunguliwa Mbeya haina zuio hivyo ni haki yao lakini vyote vinaweza kuendelea na michakato yake kwa jinsi watakavyoona wenyewe. Na kama pande mbili zitakaa tena kuongeza muda wa majadiliano basi haki itabaki chini ya serikali kwa kuamua,” amesema Silaa.
Aidha ameongeza kuwa, “Wawekezaji wengi walileta maombi yao ili wapate haki ya kuendesha bandari yetu, lakini watu wa bandari wao wanajua ni watu gani wanawahitaji kwa kuangalia vigezo na mahitaji. Makampuni yaliyoleta maombi ni Hutchson (Hong Kong), Antewerp/Brugge (Belgium),” amesema Silaa.