Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dar es Salaam, Kisutu, imeshindwa kutoa hukumu ya kesi ya aliyekuwa mhasibu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Godfrey Gugai na wenzake kutokana na kushindwa kukamilisha kuiandika hukumu hiyo.
Hukumu hiyo iliyokuwa imepangwa kutolewa leo Jumatano, Oktoba 6, 2021 Mahakamani hapo na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, amesema hajamaliza kuandika hukumu hiyo kutokana na ufinyu wa muda unaosababishwa na kukabiliwa na vikao maalum vya kesi nyingine za jinai na ukubwa wa kesi yenyewe.
Aidha Hakimu Simba amebainisha kuwa kesi hiyo ina mashahidi 42 na vielelezo zaidi ya 70, na kwamba kuvipitia vyote vinahitaji muda huku pia akieleza kuwa kwa kipindi hiki anakabiliwa na kesi nyingine za jinai za vikao maalumu ambazo bado zinaendelea.
“Kwa hiyo ndio sababu nimeshindwa kuisoma leo due to pressuer of work,” amesema Hakimu Simba na kongeza kuwa pia amechelewa kupata majumuisho ya hoja za maandishi za pande zote.
Amesema kuwa ili kupata muda wa kutosha kuiandaa hukumu hiyo anahitaji muda wa angalau siku 14 na kupelekea kesi hiyo kuhairishwa Hadi Oktoba 22, 2021 saa 5:00 adhuhuri kwaajili ya kusoma hukumi hiyo.
Mbali na Gugai washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni George Makaranga, Leonard Alloys na Yasini Katera.