Kesi ya anayedaiwa kuwa kamanda wa zamani wa kundi la Seleka wa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Mahamat Said Ablel Kani imeanza kusikilizwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC, mjini The Hague nchini Uholanzi.
Kani, anatuhumiwa kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu unaojumuisha kuwafunga watu au kuwanyima uhuru, unyanyasaji, utesaji, watu kutoweshwa na vitendo vingine vya kikatili na uhalifu wa kivita, unaojumuisha mateso na ukatili unaodaiwa kufanywa huko Bangui, mji mkuu wa CAR mwaka 2013.
Kesi hiyo, imeanza kwa Kani kusomewa mashtaka yanayomkabili na majaji watatu wanaoendesha kesi hiyo ambao ni Jaji Miatta Maria Samba, Jaji Socorro Flores Liera na Judge Sergio Gerardo Ugalde Godínez na wote kwa pamoja wameridhika kwamba mshitakiwa Said Kani, alielewa mashitaka yanayomkabili.
Mtuhumiwa Kani anayewakilishwa na wakili Jennifer Naouri amekana mashitaka yote yanayomkabili ambapo Mwendesha mashtaka wa mahakama ya ICC, Karim AA Khan KC na mwanasheria wa kesi hiyo, wakili Holo Makwaia walitoa taarifa za ufunguzi wa kesi.
Badaye, zitatolewa taarifa za ufunguzi za wawakilishi wa kisheria wa mshitakiwa ambao ni Sarah Pellet na timu yake, huku shahidi wa kwanza wa upande wa mashitaka, akipangwa kuanza kutoa ushahidi baada ya kumalizika kutolewa kwa taarifa za ufunguzi za upande wa mshitakiwa, unaotarajia kuwaita mashahidi 43 katika kesi hiyo.