Kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu imeshindikana kuendelea leo baada ya upande wa Jamhuri kusema shahidi wao wa 13 bado amepumzishwa hospitalini.

Shahidi huyo jana wakati akiendelea kuhojiwa na Wakili wa upande wa utetezi Peter Kibatala, alisimama ghafla na kuieleza Mahakama kuwa hajisikii vizuri hali iliyosababisha Jaji Joachim Tiganga anayesikiliza kesi hiyo kuiahirisha hadi leo.

Kesi hiyo ambayo ingeendelea leo Alhamisi Februari 10, 2022 kwa shahidi wa 13 wa upande wa mashtaka Mkaguzi wa Polisi, kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi, Mkoa wa Kipolisi Temeke, Tumaini Swila kuendelea kuhojiwa na upande wa utetezi.

Leo, katika mahakama hiyo Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga aliiambia Mahakama kuwa shahidi wao amepumzishwa kutokana na ushauri wa daktari wake na kuiomba Mahakama iahirishe kesi mpaka Jumatatu.

Hata hivyo, upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Peter Kibatala ulipinga ahirisho la mpaka Jumatatu wakitaka kesi hiyo kuendelea kesho Ijumaa.

Jaji Tiganga amesema amekubaliana na ombi la upande wa utetezi la kuahirisha kesi hiyo mpaka Jumatatu Februari 14 kwa kuwa suala la afya ni nyeti huku akiuagiza upande wa mashtaka kuja na shahidi huyo na kama atakuwa bado mgonjwa wapeleke shahidi mwingine.

ASEC Mimosas yaifuata Simba SC
Waziri Mkuu wa Libya anusurika kifo