Mwaka mmoja baada ya aliyekuwa mwalimu wa Shule ya Msingi Kibeta mkoani Kagera, Respicius Patrick kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa, Mahakama ya Rufani imezuia hukumu hiyo, ikiamuru kesi hiyo isikilizwe upya.

Uamuzi huo umetolewa na jopo la majaji watatu, Stella Mugasha, Lugano Mwandambo na Ignas Kitusi, baada ya kubatilisha mwenendo wa kesi hiyo kutokana na kasoro za kisheria zilizofanywa na Mahakama Kuu iliyotoa hukumu ya kifo.

Katika uamuzi wa rufaa ya mwalimu huyo, majaji hao wamesema Mahakama Kuu haikuzingatia taratibu za kisheria, katika hatua ya majumuisho, inayohusisha maoni ya wazee wa baraza.

Kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kifungu cha 265, Mahakama Kuu husikiliza kesi za jinai kwa kusaidiwa na wazee wa baraza, idadi yao ikiwa ni kuanzia wawili au zaidi kadri mahakama itakavyoona inafaa.

Dosari nyingine ni jaji kutowalezea washauri wa mahakama jambo muhimu kuhusu viambatanisho muhimu vya kosa la mauaji ya kukusudia.

Pia majaji hao wameona kuwa ingawa Mahakama Kuu ilirejea dhana ya nia ya pamoja ya washtakiwa kutenda kosa, katika muhtasari wake hakuwaelezea washauri wa mahakama maana ya nia ya pamoja kuhusianisha na kesi inayowahusisha watu wawili.

Katika uamuzi huo Mahakama ya Rufani imesema matokeo ya kasoro hizo ni kwamba wazee wa baraza hawakuelezwa barabara ili waweze kutoa maoni yao kwa usahihi.

“Kwa maneno mengine ni kwamba waliondolewa haki yao ya kueleza maoni yao kama wanavyotakiwa chini ya kifungu cha 298(1) cha CPA,”  wamesema majaji hao.

Hivyo, Mahakama ya Rufani imesema athari za tatizo hilo huufanya mwenendo wa kesi na matokeo yake, yaani hatia na adhabu, kuwa batili.

“Katika mazingira haya tunalazimika kutumia mamlaka yetu ya kimapitio tunayopewa na kifungu cha 4(2) cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa, kubatilisha mwenendo kutoka kuanza kwa usikilizwaji na tunatengua hukumu na hatia na kutupilia mbali adhabu iliyotolewa kwa mrufani,” wamesema majaji hao.

“Tunaelekeza usikilizwaji upya wa kesi dhidi ya mrufani mapema iwezekanavyo, na jaji (ahusishe) na wazee wa baraza tofauti kwa mujibu wa sheria. Mrufani ataendelea kuwa mahabusu akisubiri usikilizwaji upya wa kesi.”

Respicius, ambaye alikuwa mwalimu wa nidhamu, alihukumiwa kunyongwa Machi 6, 2019, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la mauaji ya kukusudia ya mwanafunzi wake anayeitwa Sperius Eradius.

Katika kesi hiyo namba 56, ya mwaka 2018, Mwalimu Respicius alishtakiwa pamoja na mwalimu mwenzake Herieth Gerald kwa kumuua mwanafunzi huyo Agosti 27, 2018.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Desemba 22, 2020
Baada ya miaka 400, Sayari za Jupiter na Saturn kuonekana katika umbo moja leo

Comments

comments