Kesi dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili, Silivester Nyegu na Daniel Gabriel Mbula ya unyang’anyi wa kutumia silaha imefutwa leo Julai 16,2021 iliposikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Arusha baada ya wakili Mkuu wa Serikali, Tumaini Kweka kuomba shauri hilo liondolewe mahakama hapo.
Aidha Wakili kweka ameomba shauri hilo la kesi Na 66/2021, kuhamishiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, ombi ambalo limekubaliwa na upande wa utetezi na Mahakama ambapo kesi hiyo imefutwa rasmi katika Mahakama hiyo na kuhamishiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi na kupewa kesi no 105/2021 ambapo imeanza kusikilizwa leo.
Sabaya na wenzake watano (katika mashtaka tofauti) wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Arusha leo kwa mara ya nne wakikabiliwa na mashtaka matano ya uhujumu uchumi, rushwa, kuongoza genge la uhalifu, utakatishaji wa fedha na unyang’anyi wa kutumia silaha.
Mbali na Ole Sabaya, washtakiwa wengine ni msaidizi wake wa karibu, Silvester Stanslaus, Enock Togolani, John Odemba, Daniel Gabriel Mbula, na Waston Mwakomange.