Kesi ya ubakaji inayooneshwa mubashara kwenye televisheni nchini Afrika Kusini, inayomkabili mchungaji maarufu raia wa Nigeria imezua gumzo kubwa mtandaoni lililotikisa kinachoendelea mahakamani.
Mchungaji Timothy Omotoso (60) anatuhumiwa na Cheryl Zondi (22), kuwa alikuwa akimbaka tangu alipokuwa na umri wa miaka 14 alipojiunga na huduma kanisani kwake, tuhuma ambazo mchungaji huyo amezikanusha vikali.
Katika ushahidi wake, Zondi amedai kuwa mchungaji huyo alianza kumbaka mwaka mmoja tu baada ya kujiunga na huduma ya kanisa lake akiwa miongoni mwa wasichana wanaotumikia na kusaidia kazi za kanisa. Aliiambia mahakama kuwa Omotoso alikuwa akimtishia kuwa kukataa kufanya hivyo ni kukataa kufuata ‘matakwa ya Mungu’.
Hata hivyo, maswali yaliyovurumishwa kutoka kwa mwanasheria anayemtetea mtuhumiwa yalisababisha watu kupiga kelele mahakamani mara kadhaa, huku Jaji akimzuia Zondi kujibu baadhi ya maswali hayo.
(Maswali hayo nyeti tumeshindwa kuyaandika kwa sababu za kimaadili ya jamii yetu).
Hali hiyo ilisababisha Mwanasheria wa Omotoso kumlaumu Jaji huyo kwa madai kuwa yatari ameshaoenesha kumlinda Zondi na kwamba hiyo inatokana na shinikizo kubwa lililoko kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mwenendo wa kesi hiyo.
Kesi hiyo imekuwa ya kwanza ya ubakaji kuoneshwa mubashara kwenye runinga katika nchi hiyo ambayo inaripotiwa kuwa na wastani wa matukio 100 ya ubakaji yanayoripotiwa katika vituo vya polisi kila siku.
Wengi wameendelea kuhoji kama mpango wa kuonesha kesi hiyo mubashara kwenye runinga unaweza kusaidia upatikanaji wa haki usiopendelea kutokana na huruma kwa walalamikaji au majina ya watuhumiwa.
Gumzo kubwa lililoibuka kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari nchini humo limekorezwa na mjukuu wa Nelson Mandela aitwaye Ndileka Mandela ambaye alidai kuwa yeye pia alibakwa na aliyekuwa mpenzi wake mwaka 2017, akimtia moyo Zondi kuendelea kukomaa na kuwa imara.
Baada ya maswali mazito na nyeti kutoka kwa mwanasheria anayemtetea mtuhumiwa, Jaji alimtakia mlalamikaji heri katika mitihani yake ya Chuo Kikuu ambayo ilimbidi aiahirishe kwa muda ili aweze kuhudhuria kesi hiyo.
Aidha, Jumapili iliyopita, kanisa la Mchungaji Omotoso lililopo jijini Port Elizabeth lililazimika kufungwa baada ya umati wa watu wenye hasira kulizunguka. Magazeti nchini humo pia yaliripoti kuwa mlalamikaji anadai kuwa amepokea vitisho.