Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Agosti 17 mwaka huu kuendelea na utetezi katika kesi ya kughushi inayowakabili waliokuwa viongozi wa tatu wa klabu wa Simba.
Hao ni aliyekuwa rais wa klabu, Evans Aveva na makamu wake, Godfrey Nyange pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe. Tayari mshtakiwa Aveva ameanza kujitetea na jana alitakiwa kuendelea na utetezi wake lakini, Wakili wa mshtakiwa huyo, Kung’e Wabeya alipata udhuru na hivyo ameshindwa kufika mahakamani hapo.
Kutokana na hali hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 17 itakapoendelea. Washtakiwa hao wapo nje kwa dhamana baada ya kukidhi masharti ya dhamana. Septemba 20, 2019 Mahakama hiyo iliwafutia mashtaka ya utakatishaji baada ya washtakiwa hao kuonyesha hawana kesi ya kujibu kwenye mashtaka hayo, hivyo wakawa na uwezo wa kupata dhamana.
Baada ya Hakimu Simba kusema hivyo, upande wa mashtaka walidai Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) aliwasilisha hati ya kupinga washtakiwa kupata dhamana.Katika kesi hiyo, viongozi hao wanakabiliwa na mashtaka nane yakiwemo ya kughushi.