Kesi inayowakabili viongozi wakuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe na wabunge wengine 7 imesogezwa mbele hadi Novemba 1 mwaka huu.
Kesi hiyo iliitwa leo katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu jijini Dar es salaam na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri kwa ajili ya kusikilizwa iwapo miongoni mwa washtakiwa hao ameshapata wakili wa kumuwakilisha.
Hakimu Wilbard Mashasuri amekubali ombi la kusogezwa mbele kwa kesi hiyo kufuatia wakili anayemwakilisha mtuhumiwa, Peter Msigwa kuomba muda wa kusoma nyaraka za kesi hiyo.
Aidha, Wakili, Jamhuri Joseph amedai anahitaji muda wa kutosha wa kupitia nyaraka za mteja wake ili shughuli ya kuanza kumtetea ianze mara moja mwanzoni mwa mwezi ujao.
Hata hivyo, viongonzi wakuu wa Chama hicho wanakabiliwa na makosa mbalimbali ikiwemo kosa la kuhamasisha uchochezi na kusababisha kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji Taifa (NIT) AkwIlina Akwilini wakati wa uchaguzi wa marudio katika jimbo la Kinondoni ambapo mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Maulid Mtulia alimshinda aliyekuwa mgombea wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Salum Mwalimu.