Meneja wa klabu ya Manchester City Pep Guardiola amemsifia bila kificho kiungo Kevin De Bruyne, kufuatia kazi nzuri aliyoionyesha usiku wa kuamkia leo wakati wa mchezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya  Feyenoord.

Guardiola alimwagia sifa kiungo huyo kutoka nchini Ubelgiji mbele ya waandishi wa habari, mara baada ya kikosi chake kuibuka na ushindi wa mabao manne kwa sifuri katika uwanja wa Etihad Stadium.

Meneja huyo kutoka nchini Hispania alisema, De Bruyne amekua msaada mkubwa kwenye kikosi chake na anajivunia kuwa na mchezaji wa aina hiyo.

“Kevin ni mmoja wa wachezaji bora nilionao kwa sasa, sikuwahi kuwa na mawazo tofauti dhidi yake, zaidi ya kuamini anafanya kazi kwa ajili ya kuisaidia Man City kufikia lengo la kupata ushindi kwenye kila mchezo tunaocheza, ni faraja kwangu na kwa wengine klabuni hapa.”

Guardiola pia akazungumzia umuhimu wa kikosi chake kupata ushindi kwenye mchezo wa kwanza wa ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu huu walioucheza nyumbani kwa kusema, anaamini hatua hiyo itawasaidia katika safari yao ya kupambana kwenye michezo ijayo.

“Msimu uliopita hatukubahatia kushinda michezo ya ugenini, kwa hatua hii ya kuanza kupata ushindi nyumbani naamini itatusaidia ili kufanikisha mpango wa kupambana tutakapokua nje ya Etihad Stadium ili tushinde na michezo ya ugenini.

“Tumekua na kiwango kizuri katika mchezo dhidi ya Feyenoord na tulibahatika kufunga katika dakika ya kwanza ya mchezo, hii inaonyesha safu yetu ya ushambuliaji ipo makini na tayari kwa wakati wowote kufanya kinachotarajiwa na wengi. Tuna mambo mengi ya kufanya katika michuano hii msimu huu, lakini kuanza na ushindi usiku huu ni jambo jema sana kwetu.

Mabao ya Man City katika mchezo dhidi ya Feyenoord yalifungwa na John Stones aliyefunga mawili, Sergio Aguero, Kevin de Bruyne na Gabriel Jesus.

Matokeo ya michezo mingine ya ligi ya mabingwa barani Ulaya iliyochezwa usiku wa kuamkia leo.

 

Kundi E

Liverpool 2 – 2 Sevilla

Maribor 1 – 1 Spartak Moscow

 

Kundi F

Feyenoord 0 – 4 Manchester City

Shakhtar Donetsk 2 – 1 SSC Napoli

 

Kundi G

FC Porto 1 – 3 Besiktas

RasenBallsport Leipzig 1 – 1 Monaco

 

Kundi H

Real Madrid 3 – 0 APOEL Nicosia

Tottenham Hotspur 3 – 1 Borussia Dortmund

Ni zamu ya Paris na Los Angeles Olimpiki 2024, 2028
Lema: Lissu bado yupo ICU