Kiungo wa Mabingwa wa Soka Barani Ulaya Manchester City, Kevin De Bruyne atakosa mechi za mwanzo za Ligi Kuu England msimu ujao kutokana na maumivu ya misuli ya paja yanayomsumbua.
Nyota huyo aliondolewa kipindi cha kwanza kwenye mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Inter Milan ambayo hata hivyo chama lake lilifanikiwa kubeba ubingwa kufuatia ushindi wa bao 1-0.
Kinachoonekana kwa sasa ni kwamba majeraha hayo yalikuwa siriazi na atachelewa kuripoti kambini kwa muda uliopangwa hadi atakapokuwa fiti.
Kiungo huyo wa kimataifa wa Ubelgiji alipata maumivu makali ya misuli ambayo yatamfanya akose mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Arsenal kabla ya ligi kuanza.
Vilevile atakosa mechi ya kwanza ya ligi dhidi ya Burnley ambayo ilipanda daraja msimu uliopita watakayokipiga ugenini kwenye Uwanja wa Turf Moor.
Madaktari wa Manchester City wanaamini kwamba De Bruyne anaweza kurejea kwenye mechi ya Super Cup dhidi ya Sevilla itakayocheza baadaye.
Taarifa nzuri ni kwamba kiungo huyo hatafanyiwa upasuaji na kama mambo yatakwenda kama ilivyo haitaathiri kiwango chake msimu ujao.
Taarifa zimeripoti kwa sasa De Bruyne aliambiwa apumzike pamoja na familia yake kabla ya matibabu yake mwezi ujao. Hivi karibuni kiungo huyo alionekana akila bata na wachezaji wenzake kina Nathan Ake na Virgil van Dijk.
Wakati huohuo Man City imekamilisha usajili wa Mateo Kovacic aliyejiunga akitokea Chelsea.
Kiungo huyo amesajiliwa kwenda kuziba pengo la Ilkay Gundogan ambaye tayari amejiunga na FC Barcelona.