Kiungo kutoka nchini Ubelgiji na Klabu ya Manchester City, Kevin de Bruyne ameipa hofu klabu hiyo baada ya kuumia goti kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya FC Bayern Munich.

Kiungo huyo alishindwa kumaliza mchezo huo na kufanyiwa mabadiliko nafasi yake ikachukuliwa na Julian Alvarez katika dakika ya 68.

Jeraha la De Bruyne lilikuja baada ya kiungo huyo kujaribu kuokoa mpira kwa kutumia mguu wa kulia na Man City ikaingiwa hofu alipoanguka.

Madaktari wa timu hiyo waliingia uwanjani na kumpatia matibabu haraka lakini ililazimu kumtoa.

Mashabiki wa Man City walipata presha baada ya kiungo huyo muhimu kuumia katika mchezo ambao waliibuka na ushindi wa mabao 3-0 kwenye mchezo huo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi Mabingwa Ulaya.

Shabiki mmoja aliandika kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter akisema ana matumaini jeraha la De Bruyne sio kubwa na atakuwa freshi kwa ajili ya mechi nyingine zinazofuata.

Hata hivyo, shabiki mwingine alionyesha hofu akisisitiza: “Tafadhali De Bruyne usiumie hata kama hukucheza kwa kiwango bora dhidi ya Bayern.”

Shabiki wa tatu alisema endapo jeraha la De Bruyne litakuwa kubwa itakuwa pigo kubwa kwao kwa sababu bado wana mechi muhimu kuelekea katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England.

Naye shabiki wa nne akamalizia kwa kusema, “Julian Alvarez aliingia kuchukua nafasi ya De Bruyne, matumaini yangu kiungo wetu hajaumia sana.’

Mabao ya Manchester City dhidi ya Bayerm yaliwekwa kimiani na Rodri katika dakika ya 27, Bernardo Silva dakika ya 70, huku Erling Haaland akishindilia msumari wa mwisho katika dakika ya 76.

Ashikiliwa kwa kuchoma moto Maduka alipwe Bima
Elias Maguri mambo safi Geita Gold FC