Kiungo kutoka nchini Ubelgiji na Klabu ya Manchester City, Kevin De Bruyne huenda akakaa nje ya dimba kwa kipindi kisichopungua miezi miwili baada ya kupata majeraha ya misuli katika mchezo wa Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, dhidi ya Inter Milan, uliopigwa Jumamosi (Juni 10) mjini Istanbul, Uturuki.

De Bruyne alilazimika kutolewa katika dakika ya 35 ya mchezo huo, baada ya kupata majeraha ambapo bao pekee lililoipa ubingwa City lilipachikwa wavuni na Rodri katika dakika ya 68.

Kiungo huyo amesema alipata majeraha ya misuli ambayo yatamfanya akae nje ya dimba kwa muda ili kuhakikisha anarejea katika hali yake ya kawaida.

“Nilifanya kila kitu katika msimu huu ili kuhakikisha timu inafanya vizuri, ninajivunia mafanikio makubwa iliyopata timu yangu kwani na mimi nilichangia kwa kiasi kikubwa.

“Hakuna kibaya kilichotokea, kila mmoja alijitahidi kutimiza majukumu yake kwa manufaa ya klabu na mashabiki kwa ujumla.

“Nimepata majeraha na tayari nimeambiwa ninaweza kukaa nje ya dimba kwa kipindi kisichopungua miezi miwili, ninaamini nitarejea msimu ujao nikiwa na kiwango bora.

“Kuna baadhi ya mechi ambazo nilizikosa kutokana na changamoto mbalimbali zikiwemo za familia, lakini mechi dhidi ya Arsenal, Bayern (Munich) na (Real) Madrid nilicheza kwa kiwango bora na kutoa mchango wangu ndani ya timu.

“Kuna wakati nilikabiliwa na changamoto za kifamilia badae nilizitatua na kutimiza majukumu yangu kikosini,” amesema staa huyo.

Wakulima wawezeshwe ili wazalishe kwa wingi - Othman
Ujumuishi ni nguvu: Tuwape nafasi kukomesha ukosefu wa usawa