Baada ya kusikia Manchester City inafikiria kumpiga bei kiungo wake kutoka nchini Ubelgiji Kevin de Bruyne katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi, taarifa zinadai matajiri wa Saudi Arabia wameanza kupigana vikumbo.

De Bruyne ambaye ameshinda taji la Ligi Kuu England mara tano akiwa na matajiri hao wa Jiji la Manchester, mkataba wake unamalizika mwaka 2025 na hadi sasa Man City haijakaa mezani na wawakilishi wake juu ya kujadili mkataba mpya.

Kwa sasa kiungo huyu wa kimataifa wa Ubelgiji anasumbuliwa na majeraha na atakuwa nje hadi mwakani hali ambayo pia imesababisha vigogo wa Man City kusita kumsainisha mkataba mpya.

Mpango wa Wasaudia ni kumchukua fundi huyu mwisho wa msimu huu ambapo mkataba wake utakuwa umebakisha msimu mmoja kumaizika.

Mshahara wake sasa ni Pauni 400,000 kwa juma na City imepanga kumpunguzia ili kumsainisha dili jipya, huku Waarabu wakipanga kumuongezea zaidi.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 32, msimu uliopita alicheza mechi 49 za michuano yote, akafunga mabao na kutoa asisti 31.

Bakari Shime: Tutamalizia kazi Botswana
Wamasai Kenya wampa masharti Mfalme Chalres