Klabu ya Società Sportiva Lazio ya Italia huenda ikamsajili mlanda mlango wa Real Madrid Keylor Navas itakapofika mwishoni mwa msimu huu.
Gazzetta dello Sport limeripoti kuwa, mlinda mlango huyo kutoka Costa Rica amekua akifuatiliwa kwa ukaribu na viongozi wa Società Sportiva Lazio na tayari baadhi yao wameonyesha kuridhishwa na uwezo wake.
Mkurugenzi wa michezo wa Società Sportiva Lazio Igli Tare na Rais Claudio Lotito, juma lililopita walihudhuria Estadio Stantiago Bernabeu kushuhudia mchezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya ambapo Real Madrid walipambana na Società Sportiva Calcio Napoli.
Lengo la usajili wa mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 30, ni kutaka kumpa changamoto kipa chaguo la kwanza la Lazio Federico Marchetti.
Ufuatiliaji wa kiwango cha mlinda mlango huyo, umeanzishwa na viongozi wa Lazio kutokana na uhakika uliwahi kutangazwa na Rais wa klabu ya Real Madrid Florentino Perez wa kumuuza Navas itakapofika mwishoni mwa msimu huu.