Kiungo kutoka nchini Uganda Khalid Aucho huenda akaukosa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC, utakaopigwa Jumatano (April 06) saa moja kamili usiku katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi, jijini Dar es salaam.
Kiungo huyo aliyesajiliwa Young Africans mwanzoni mwa msimu huu, anatajwa kuwa kwenye hatari wa kuukosa mchezo huo, kufuatia kujitonesha jeraha la misuli ambalo limemuweka nje kwa majuma kadhaa.
Kocha Msaidizi wa Young Africans, Mrundi, Cedric Kaze, amesema kuwa Aucho yupo katika hatihati ya kuwepo kwenye mchezo dhidi ya Azam FC baada ya kujitonesha maumivu ya misuli.
Kaze amesema kuwa benchi lao la ufundi limepata taarifa hizo hivi karibuni za kiungo huyo kujitonesha akiwa katika kambi ya timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’.
Ameongeza kuwa wakati Aucho akiwa katika hali ya hatari kuukosa mchezo dhidi ya Azam FC, Benchi la Ufundi la klabu hiyo linafurahia kuona baadhi ya wachezaji waliokuwa majeraha wanarejea ambao ni Shomari Kibwana na Chrispin Ngushi ambao walicheza mchezo wa kirafiki uliopita dhidi ya Mafunzo FC ya Zanzibar.
“Kiungo wetu Aucho aliitwa kwenye timu ya taifa ya Uganda akiwa hajapona vizuri na baada ya mazoezi na timu yake ya taifa juzi alijitonesha eneo lilelile.”
“Na timu ya taifa haijampatia vipimo kujua tatizo lake hivyo leo Alhamisi (jana) atarejea nchini na kufanyiwa vipimo ili kujua ukubwa wa tatizo lake.
“Huyo atakuwa kiungo wetu wa pili muhimu katika timu huenda akaukosa mchezo ujao wa ligi dhidi ya Azam FC, mwingine ni Fei Toto ambaye yeye amepewa mapumziko ya majuma mawili kutokana na jeraha la goti,” amesema Kaze ambaye aliwahi kukinoa kikosi cha Young Africans kama Kocha Mkuu kabla ya kufukuzwa msimu uliopita na msimu huu alirudi na kukabidhiwa jukumu la kuwa msaidizi wa Kocha Nabi.
Young Africans inajiandaa kuikabili Azam FC, huku ikiongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 48 zilizooatikana katika michezo 18 waliocheza, huku zikiweka tofauti ya alama 11 dhidi ya Mabingwa watetezi Simba SC inayoshika nafasi ya pili kwa kuwa na alama 37, baada ya kucheza michezo 16.
Azam FC ipo nafasi ya tatu ikiwa na alama 28 zilizopatikana baada ya timu hiyo kucheza michezo 18 hadi sasa.