Kinda la klabu ya Azam FC Khelffin Hamdoun, limekosa nafasi ya kusajiliwa kwenye kikosi cha vijana cha Liverpool ya England, baada ya kupita kwenye majaribio aliyofanyiwa na jopo la makocha wa timu za vijana za klabu hiyo.
Taarifa kutoka Azam FC zimeeleza kuwa, kinda hilo kutoka Visiwani Zanzibar lilikwenda England mwezi uliopita, na lilifanikiwa kuwavutia makocha wa Liverpool, lakini kilichomkwamisha katika usajili ni kufungwa mapema kwa dirisha la usajili.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Azam FC Thabiti Zakaria amesema kuwa: “Ni kweli Khelffin yupo Liverpool kwa ajili ya majaribio, ameweza kupita lakini shida imekuja usajili wa Liverpool umeshafungwa.”
“Atarejea nyumbani mpaka usajili wa dirisha dogo utakapofunguliwa, Inshaallah ataenda tena.”
Khelffin Hamdoun alisajiliwa Azam FC mwaka 2020 akitokea Mlandege ya Zanzibar, baada ya kuonesha kiwango kikubwa cha soka kupitia michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambayo hufanyika kila mwaka.