Aliyekua kiungo wa klabu ya Swansea City iliyoshuka daraja nchini England kutoka ligi kuu hadi ligi daraja la kwanza, Ki Sung-yueng amejiunga na Newcastle United kwa mkataba wa miaka miwili.

Ki ambaye alikua nahodha wa kikosi cha Korea kusini wakati wa kusaka nafasi ya kushiriki fainali za kombe la dunia, na baadae kupokwa unahodha walipofika nchini Urusi, amekamilisha dili hilo kwa kusaini mkataba wa miaka miwili.

Ki, anaondoka Swansea City baada ya kuitumikia kwa muda wa miaka sita ambapo alifanikiwa kufunga mabao 12 katika michezo 160 aliyocheza.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 29, amepata nafasi ya kuondoka klabuni hapo kwa urahisi, kufuatia hitaji lake la kutaka kucheza katika ligi kuu ya England, kutokana na Swansea kushuka ndaraja msimu uliopita, baada ya kumaliza katika nafasi ya 18 kwenye msimamo wa ligi.

“Ni kama ndoto kwangu kufanikisha jambo hili, nilikua na malengo ya kucheza katika uwanja wa St. James’ Park mara kwa mara, tulikuja hapa mara kadhaa katika michezo ya ligi, lakini kwa sasa ndio mahala pangu pa kazi, nimefurahi sana,” alisema Ki baada ya kukamilisha usajili wake.

“Kila mmoja anafahamu ukubwa na umuhimu wa Newcastle Utd katika ligi ya England, ninatambua nimejiunga na klabu yenye malengo yenye kuendelea, ninatarajia ushirikiano mkubwa kutoka kwa wachezaji wenzangu ili tufanikishe kilichokusudiwa kwa msimu huu,” aliongeza kiungo huyo.

Mkataba wa Ki na Newcastle Utd utaanza rasmi Julai Mosi, na anakua mchezaji wa pili kusajiliwa katika kipindi hiki baada ya mlinda mlango Martin Dubravka, kusaini mkataba wa muda mrefu na klabu hiyo, baada ya kusajiliwa kwa mkopo miezi sita iliyopita, akitokea Sparta Prague ya Jamuhuri ya Czech.

Ki alicheza fainali za kombe la dunia zinazoendelea nchini Urusi dhidi ya Sweden na Mexico, lakini alikosa mchezo wa mwisho dhidi ya Ujerumani ambao walichomoza na ushindi wa mabao mawili kwa sifuri, kufuatia jeraha la kiazi cha mguu.

Majibu ya tathmini yawabeba Giorgio Chielini, Andrea Barzagli
Diego Maradona aombwa kutunza heshima yake