Mchezaji na Kocha Mkuu wa zamani wa Simba SC, Abdallah King Kibadeni, amewataka Wanachama na Mashabiki wa klabu hiyo kuheshimu maamuzi ya Kocha Mkuu, Robertinho Oliveira, kutokana na kumtupia lawama kwa kutomchezesha straika Mzambia Patrick Phiri.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Kibadeni anayeshikilia rekodi ya kufunga mabao matatu Hat-Trick, kwenye mechi ya watani wa jadi ‘dabi’ ya Simba SC na Young Africans, amesema mashabiki wanamkosea kocha huyo kwani kitendo cha kumlazimisha kumchezesha ni kama vile wanamuingilia kwenye majukumu yake.
“Kitendo cha Wanachama na Mashabiki wa Simba SC kumshutumu kuwa hamchezeshi Phiri ni kama kumuingilia kwenye majukumu yake, yeye ndiye anayekaa na wachezaji na anawajua nani anatakiwa kucheza mechi hii na nani asubiri acheze lini, hii kulazimika kupangwa mchezaji kwa lazima si sawa sawa kabisa,” amesema Kibadeni.
Mara baada ya Tamasha la Simba Day, ingawa alitambulishwa na kuonekana akipungia mashabiki kwenye orodha wachezaji 30, lakini hakucheza mechi hiyo, ikiwa ni mfululizo wa kutoonekana kwake uwanjani tangu msimu uliopita huku ikidaiwa kuwa ameshapona majeraha yaliyokuwa yanamkabili.
Kibadeni amesema hakuna kocha yeyote anayeweza kumuacha mchezaji mzuri nje au kupangiwa cha kufanya kwa sababu hata yeye anahitaji ushindi kuliko mtu yeyote na timu ikipoteza wao ndiyo hubeba lawama.
“Sisi makocha timu ikifungwa ndiyo tunabeba lawama kwa hiyo hakuna anayetaka kupoteza mechi kwa ajili ya kumuweka mchezaji mzuri nje, nadhani wawe wavumilivu tu kwa sababu anachokifanya na kukiona ni sahihi kwake kwa sasa na nadhani Simba SC ina mashindano mengi hakuna mchezaji atakayeweza kucheza mechi zote hizo. Najua atacheza tu wasiwe na haraka,” amesema kocha huyo ambaye pia alikuwa mmoja wa makocha walioifikisha Simba SC fainali ya Kombe la Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) mwaka 1993 akiwa chini ya Kocha Mkuu, Muethiopia Etienne Eshete.
Wanachama na Mashabiki wa klabu hiyo licha ya kumshambulia kocha huyo kwenye mitandao ya kijamii, baadhi yao wamedai huenda kocha huyo anapata shinikizo kutoka kwa baadhi ya viongozi.
Mpaka sasa hakuna kiongozi yeyote wa Simba SC, wala Meneja Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally, aliyetaka kulizungumzia suala hilo ingawa kwenye akaunti yake yake ya instagram, baadhi ya mashabiki wamemwandikia kuwa kama kuna tatizo na mchezaji huyo walitatue haraka sana kwa sababu haileti taswira nzuri kwenye klabu.
Phiri aliyesajiliwa mwanzoni mwa msimu uliopita kutoka Zanaco FC ya nchini kwao Zambia, aliumia katika mechi ya Ligi Kuu Desemba 21, mwaka jana kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba mkoani Kagera, timu hizo zikitoka sare ya bao 1-1 na kukaa kwa muda mrefu akijiuguza.
Amecheza mechi chache hasa za Ligi ya Mabingwa akiingia kipindi cha pili kitu ambacho kinaashiria kuwa amepona, lakini amekuwa si sehemu ya kikosi cha Robertinho kwenye mechi nyingi za mwisho za Ligi Kuu msimu uliopita.