Simba SC imemaliza ubishi kwa kushinda pambano la 110 la Ligi Kuu Bara tangu kuasisiwa kwa ligi hiyo mwaka 1965, lakini bado Rekodi ya Hat trick ya Abdallah Kibadeni ‘King’ imeshindwa kuvunjwa kwenye michezo ya watani wa jadi.
Kibadeni alifunga Hat Trick kwenye pambano lililopigwa Julai 19, 1977 wakati Simba SC ikiifumua Young Africans kwa mabao 6-0 na imeshindwa kuvunjwa wala kufikiwa kwa muda unaokaribia miaka 46 licha ya Simba SC na Young Africans kuwa na Washambuliaji walioweka heshima kubwa kwa kutu- pia mipira kambani.
Katika mchezo huo uliyokuwa wa 1l, ulipigwa Siku ya Jumanne, Kibadeni alifunga mabao yake dakika za 10, 42 na 89, huku Jumanne Hassan ‘Masimenti’ akifunga mengine mawili katika dakika za 60 na 73, na Young Africans Selemani Sanga akijifunga dakika ya 20.
Mchezo huo unaoshikilia Rekodi ya kuwa kipigo kikali zaidi kwa watani, ilikuwa ni ya kulipa kisasi kwani Juni Mosi, 1968, Simba SC iliifumua Young Africans kwa mabao 5-0, ingawa Mei 6, 2012 Yanga ilinyukwa tena mabao 5-0 na Simba SC.
Kumalizika kwa pambano hilo bila rekodi ya Kibadeni kuvunjwa inafanya Simba SC na Young Africans kwa msimu huu kusubiri majaliwa ya kukutana tena fainali ya ASFC kama zitapenya kwenye michezo yao ya Nusu Fainali dhidi ya Azam FC na Singida Big Stars, ili kuona kama wataifika, vinginevyo kwenye ligi ni hadi msimu ujao, kwani mchezo wa kwanza baina yao uliisha kwa sare ya 1-1 Oktoba 23, mwaka 2022.