Serikali kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) inatarajia kuanza kufanya kazi ya usanifu wa ujenzi wa Barabara ya njia nne kutoka Kibaha -Chalinze -Morogoro hadi Segera.
Afisa Sayansi ya Jamii Mkuu kutoka TANROADS Makao Makuu, Gibson Mwaya, ametoa taarifa hiyo leo Mjini Kibaha katika kikao maalum kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge.
Mwaya amesema kazi hiyo itaanza mapema wiki ijayo na kusisitiza kuwa kazi ya usanifu wa ujenzi wa Barabara hiyo itafanyika kwa muda wa miezi miwili na baadae ripoti ya awali itakabidhiwa kwa Mtendaji Mkuu.
Ameongeza kuwa baada ya kumaliza usanifu huo ripoti hiyo itaeleza namna ambavyo kazi inapaswa kufanyika pamoja na gharama halisi za ujenzi wa Barabara hiyo.