Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), limemwandikia barua Rais Dkt. Magufuli ya kuomba kukutana naye ili wampe ushauri wa mchakato wa kupatikana kwa kwa Katiba mpya.
Hayo yamesemwa Jijini Dar es salaam na Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Deus Kibamba, ambapo amesema kuwa wanakusudia kumweleza na kumshauri Rais Magufuli umuhimu wa mahitaji ya kupatikana kwa Katiba mpya kuliko wakati mwingine wowote ili imsaidie katika kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
“Unaposema unanyoosha nchi sawa, lakini hatuwezi kunyoosha nchi kwa kamba au kwa pima maji,nchi inanyooshwa kwa Katiba,inawezekana kwamba ni suala la bahati mbaya kwa washauri wa Rais kuhusu Katiba na sheria hawajafanya kazi yao sawa sawa kuhusu hili,”amesema Kibamba.
Aidha, kuhusu mkutano mkuu wa kitaifa, amesema kuwa utajumuisha asasi mbalimbali za kiraia,Serikali na wasomi waliobobea katika michakato ya kidemokrasia kutoka nje na ndani ya nchi na watafanya uchambuzi na kutoa ushauri wa mwelekeo mpya wa hapa tulipo.
Hata hivyo, Kibamba amesema kuwa wanamuomba Rais Magufuli avunje ukimya kwa kuwaeleza watanzania mwelekeo wa kupata Katiba mpya kabla ya robo ya mwaka huu haijaisha.