Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC Imani Kajula amesema Klabu hiyo juma hili itafanya Mnada wa Kibegi pamoja na Jezi zilizozinduliwa kileleni mwa Mlima Kilimanjaro mwishoni mwa juma lililopita.
Kajula amefichua mpango huo alipozungumza na Waandishi wa Habari mapema leo Jumanne (Julai 25) jijini Dar es salaam, huku akisema zoezi hilo ni sehemu ya matukio yatakayofanyika katika Wiki ya Simba ambayo rasmi itazinduliwa Jumamosi (Julai 29).
Amesema fedha zitakazopatikana katika zoezi hilo la Mnada zitasaidia ujenzi wa Wodi ya kina mama na mtoto kwenye hospitali ya Muhimbili na Zanzibar.
“Wiki ya Simba ni wiki ya kurudi kwa jamii, wiki ya kutambulisha wachezaji wapya kwa mashabiki wetu, Simba kutoa misaada kwa watu wenye uhitaji na kuchangia damu.”
“Kambi ya Uturuki inaendelea vizuri.”
“Wiki hii tunatarajia kufanya mnada wa kibegi pamoja na jezi zile na mapato yake yatasaidia ujenzi wa wodi ya kina mama na mtoto kwenye hospitali ya Muhimbili na Zanzibar.”
“Niwashukuru washirika wetu wakubwa wa Simba Week na Simba Day, CRDB Bank lakini pia kuna washiriki wengine wakubwa wataingia.” “Wiki ya Simba tumeibatiza kuwa ni wiki ya UNYAMA MWINGI. SIMBA WEEK, UNYAMA MWINGI, SIMBA DAY, UNYAMA MWINGI. Unyama Mwingi inawasilisha mambo mengi ambayo yatatokea ndani ya wiki hii.” Amesema Imani Kajula