Kiungo Mshambuliaji wa Simba SC, Kibu Denis ameahidi kuwapa furaha mashabiki wa timu yake katika mchezo wa Mkondo wa Pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos.

Kikosi cha Simba SC kipo kambini kujiandaa na mchezo huo utakaopigwa Oktoba Mosi, Uwanja wa Azam Complex huku miamba hiyo ya Tanzania ikihitaji sare isiyozidi 1-1 au ushindi wa aina yoyote kutinga hatua ya makundi.

Akizungumza jijini Dar es salaam, mchezaji huyo amesema mbinu wanazopewa na Kocha wao mkuu, Roberto Oliveira “Robertinho na dhamira waliyonayo ndiyo inamfanya awe na matumaini hayo.

“Ni mchezo mgumu ambao umebeba matumaini ya kucheza hatua ya makundi, kila mchezaji anajua umuhimu wa ushindi, binafsi nimejiandaa vizuri kuifungia timu yangu bao muhimu la kuivusha,” amesema Kibu.

Kibu amesema pamoja na matokeo ya mchezo wa kwanza kuwa mazuri kwao lakini katika mchezo wa Jumapili wamedhamiria kupambana ili kupata ushindi.

Amesema kocha wao amewapa mbinu bora zitakazowawezesha kupata ushindi hivyo amewaomba mashabiki wa Simba SC kufika uwanjani kwa wingi ili kushuhudia wakifuzu hatua ya makundi kwa msimu wa tano.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Levy Mwanawasa, Zambia Simba SC ililazimisha sare ya mabao 2-2 mabao yote ya Mnyama yakifungwa na Clatous Chama.

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Septemba 27, 2023
Awesu: Hatuna mipango ya ubingwa 2023/24