Wakati aliyekuwa kocha mkuu wa Simba SC, Roberto Oliveira ‘Robertinho’, anatua Msimbazi, alimtaja Kibu Denis kuwa mmoja wa wachezaji bora zaidi ndani ya kikosi hicho na kumpa zawadi, na baada ya hapo kazi iliendelea huku staa huyo akitakata katika utawala wake.

Kibu chini ya Robertinho alikuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza na kuweza kuonyesha ubora wake uliowakosha mashabiki na wadau wa soka waliomchukulia poa mwanzo, lakini baada ya kuondoka kwa kocha huyo baadhi ya mashabiki wamekuwa na wasiwasi juu ya uwezo wa mshambuliaji huyo huku yeye akisema waondoe shaka.

Kibu ambaye amejumuishwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’ inayojiandaa na mechi za kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Niger na Morocco, amesema anaamini katika uwezo wake na siyo kubebwa kama wengi wanavyodhani.

“Siamini kwenye kubebwa, bali kupambana na kuonyesha kitu kila ninapopata nafasi,” amesema Kibu na kuongeza: “Soka ni mchezo wa wazi na kila mtu anaona, hivyo sitaki kuongea mengi kwani kazi yangu ni kucheza na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi, hivyo naamini nitaendelea kufanya hivyo kila nikipata nafasi.”

Kibu anamudu kucheza winga zote mbili na eneo la ushambuliaji wa kati, ambapo katika msimu huu ameihusika kwenye mabao matatu ya Simba SC katika Ligi Kuu akifunga moja na kutoa pasi za mwisho ‘asisti’ mbili.

Kibu alijiunga na Simba SC akitokea Mbeya City Mwanzoni mwa msimu uliopita lakini kabla ya hapo aliwahi kuzichezea klabu za Geita Gold na Kumuyange FC.

Madiwani Chalinze wapitisha wazo la Nyota tano
Simba SC yakiri mambo magumu Ligi Kuu