Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Kibu Denis, amepanga kutoshangilia endapo ataifunga Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa baadae leo Jumatatu (Januari 17), Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Kibu Denis ametoa ahadi hiyo, kufuatia heshima aliyoipata kwenye klabu ya Mbeya City ambayo aliwahi kuitumikia kabla ya kusajiliwa kwa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC mwanzoni mwa msimu huu.
Mshambuliaji huyo amesema maisha ya upendo aliyoishi kwenye klabu ya Mbeya City msimu uliopita, ndio chanzo cha msukumo wa kutarajia kufanya uungwana wa kutoshangilia endapo ataifunga klabu hiyo.
“Nikifunga goli katika mchezo wetu na Mbeya City, Sitashangilinia kwa kuwa nilikuwepo hapa msimu uliopita na niliishi vizuri na kila mmoja.” amesema Kibu Denis
Mbeya City ilimsajili Kibu Denis mwanzoni mwa msimu wa 2020/21 akitokea Geita Gold FC iliyokua ikishiriki Ligi Daraja la Kwanza kwa wakati huo, na alionesha kiwango kikubwa kwa kupachika mabao muhimu klabuni hapo kabla ya kutimkia Simba SC.