Habari njema kwa Mashabiki na Wanachama wa Simba SC kuhusu kiungo wao Denis Kibu amepata nafuu ya majeraha yake na Jumapili (Novemba 05) atakuwepo katika mchezo wa Kariakoo Dabi.
Kibu anakumbukwa na Young Africans baada ya msimu uliopita ambao Simba SC ilishinda 2-0, kiungo huyo alifunga bao la pili. Lingine litifungwa na Henock Inonga.
Kiungo huyo alipata maumivu ya misuli katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ihefu FC na kusababisha ashindwe kuendelea na mechi hiyo.
Skudu afunguka ishu ya kusugua benchi
Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira Mbrazili, ‘Robertinho’ amesema Kibu yupo fiti kucheza dabi baada ya kupona kwa asilimia mia moja.
Robertinho amesema kiungo huyo mara baada ya kupata maumivu, haraka alipatiwa huduma ya kwanza uwanjani baada ya kutolewa nje.
“Kibu amepata nafuu ya maumivu yake ambayo yalimsababishia ashindwe kuendelea na mchezo uliopita wa ligi dhidi ya Ihefu tuliyocheza nayo Jumamosi (Oktoba 28) Uwanja wa Mkapa.
“Sasa anatarajiwa kuwa miongoni mwa wachezaji watakaocheza mchezo dhidi ya Young Africans, baada ya kupata nafuu ya maumivu ambayo hayakuwa makubwa sana ya kusababisha ashindwe kucheza.
“Ni kati ya wachezaji walioingia kambini tangu jana Jumatatu (Oktoba 30), kujiandaa na dabi hiyo ambayo kwetu tunahitaji ushindi na sio kitu kingine,” amesema Robertinho.