Beki wa Pembeni wa Young Africans Shomari Kibwana ameweka wazi mipango na mikakati wa kikosi cha klabu hiyo kwa msimu huu 2021/22, huku michezo kadhaa ikisalia kabla ya kufikia ukingoni.
Shomari ambaye kwa sasa ni gumzo katika Soka la Bongo kufuatia kuonyesha uwezo mkubwa wa kucheza Beki wa Pembeni pasina kuchagua upande, amesema dhamira kubwa ya Young Africans kwa msimu huu ni kumaliza msimu bila kupoteza mchezo sambamba na kutwaa ubingwa.
Beki huyo aliyesajiliwa Young Africans akitokea Mtibwa Sugar, amesema kila mchezaji ndani ya klabu hiyo anafahamu wajibu wake na ndio maana kila wanapokua kwenye mapambano ya kuwania alama tatu za kila mchezo huwa wanakua makini.
“Kikubwa mpaka sasa kwanza atuhitaji kupoteza mchezo wowote na ili tusipoteze tunahitaji kucheza mechi bila kuruhusu goli kwa kila mchezo, sisi kama walinzi wa timu tupo tayari kwa ajili ya kupambana ili kutimiza malengo yetu.” Amesema Shomari Kibwana.
Young Africans leo Jumatano (Mei 04), itacheza mchezo wa Mzunguuko wa 22 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting katika Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.
Klabu hiyo yenye maskani yake makuu katika makutano ya Mitaa ya Twiga na Jangwani jijini Dar es salaam, inaendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikishja alama 55, ikiwaacha Mabingwa watetezi Simba SC kwa alama 12.