Mshambuliaji kutoka nchini misri na klabu ya Liverpoool, Mohamed Salah amesema kufungwa 1-0 na Inter Milan katika mchezo wa mkondo wa pili wa Hatua ya 16 Bora wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, kutakuwa kama “simu” ya kuwaamsha ili wajitume zaidi kwa ajili ya kutinga fainali.
Wakiwa wanaongoza 2-0 katika mchezo wa mkondo wa kwanza kutokana na mabao ya Roberto Firmino na Salah dakika za lala salama, Wekundu hao walionekana kustarehe katika saa ya kwanza ya mchezo wa mkondo wa pili uliyochezwa juzi Jumanne (Machi 08) kwenye Uwanja wa Anfield.
Lakini bao la kwanza la Lautaro Martinez kwenye mashindano hayo tangu Novemba mwaka juzi, liliwapa Inter matumaini makubwa ya angalau kulazimisha muda wa ziada.
Kadi nyekundu ya Alexis Sanchez sekunde 107 baadaye ilionekana mbaya, ingawa, Inter ilishindwa kutengeneza nafasi nyingine za wazi.
Kipigo hicho ni cha kwanza kwa Liverpool katika dimba la Anfield katika michuano yote tangu Machi 7, mwaka jana.
Lakini kwa kuwa timu yake imefanya vya kutosha kuendeleza ushindi wa 2-1 kwa jumla, Salah ana matumaini ya kutumia kipigo hicho kama ishara ya kuwaamsha.
“Ni timu ngumu,” Salah aliiambia BT Sport. “Hata katika mchezo wa ugenini walikuwa wazuri sana, tulipambana mwanzoni. Tulikuwa na mpira kipindi cha pili zaidi.
“Kitu muhimu ni kufuzu, kikubwa ni timu kufuzu, tumepoteza mchezo lakini ni mchezo mzuri kwetu kuuchukua na kujifunza.
“Labda tulijiamini kupita kiasi. Siku zote ni muhimu kushinda, lakini usiku wa leo (juzi) tumegonga nguzo mara mbili, na kukosa nafasi.
“Kila mtu anataka kushinda Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ligi Kuu, kwa hiyo tutapigania zote mbili.”