Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya ilionekana kama majibu sahihi ya kuwa uamuzi wa FC Bayern Munich kuachana na Kocha Julian Nagelsmann na kumchukua Thomas Tuchel hayakuwa sahihi na walikurupuka.
Hiyo ni baada ya kufungwa mabao 3-0 katika Ligi ya Mabingwa mbele Manchester City Jumanne (April 11) na kuwafanya City kuweka mguu mmoja katika nusu fainali ya michuano hiyo.
Hata hivyo kabla ya City kufanya matokeo kuwa 2-0, UEFA iliandika maoni katika dakika ya 74 ambayo yalionesha wazi kuwa Tuchel anateseka akiwa na Bayern ambao walipaswa kuwa na subira kwa kocha Nagelsmann.
Nagelsmann alitimuliwa mwezi uliopita Bayern baada ya kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Bayer Leverkusen kwenye Bundesliga.
Mkufunzi wa zamani wa Chelsea, PSG na Borussia Dortmund, Tuchel, 49, aliteuliwa kuchukua nafasi yake na mambo yanaonekana kwenda kombo ndani ya muda mfupi tu.