Maofisa wa Manchester United tayari wana wasiwasi kuhusu kumaliza katika nafasi nne za juu msimu huu, baada ya kufungwa na Manchester City, kwa mujibu wa ESPN.
Ushindi wa mabao 3-0 wa Man City katika Uwanja wa Old Trafford Jumapili (Oktoba 29), uliiacha United katika nafasi ya nane kwenye msimamo pointi l1 nyuma ya vinara Tottenham Hotspur na pointi nane nyuma ya nafasi za Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Imezua hofu ndani ya klabu hiyo kwamba wanakabiliwa na msimu mwingine nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kushindwa kufuzu mara nne katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Kwa mujibu wa ESPN United bado wana imani kwamba kocha, Erik ten Hag, anaweza kubadilisha mambo, ingawa kuna kukubalika kwamba kiwango kitahitaji kuboreshwa sana ikiwa wanataka kumaliza katika nafasi nne za juu msimu huu.
United leo Jumatano (Novemba Mosi) itacheza na Newcastle United kwenye Kombe la Carabao kabla ya mechi za ugenini dhidi ya Fulham na FC Copenhagen kwenye Ligi ya mabingwa.
Mchezo wao wa mwisho kabla ya mapumziko ya kimataifa ya Novemba ni dhidi ya Luton Town katika Uwanja wa Old Trafford.
Chanzo kimoja kiliiambia ESPN kwamba United wana matumaini ya kuwa na Aaron Wan-Bissaka kabla ya mapumziko baada ya kukosa mechi tisa zilizopita kutokana na jeraha la misuli ya paja huku Casemiro, ambaye alikosa mechi ya ‘Manchester Dabi’ kutokana na tatizo la kifundo cha mguu, pia anakaribia kurejea.