Kiungo mshambuliaji Shiza Kichuya, amewataka mashabiki Namungo FC, kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho timu yao inapitia wakati mgumu kwa kupata matokeo mabovu, kwenye michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Namungo FC imepoteza michezo miwili mfululizo dhidi ya Polisi Tanzania FC ksha Tanzania Prisons yote ikipoteza kwa kufungwa bao moja kwa sifuri, huku wakianza vyema kwa kuifunga Coastal Union bao moja kwa Sifuri Septemba 06.

Kichuya amesema Namungo FC itarejea kwenye makali yake kutokana na uhakika na uhodari wa kocha wao Hitimana Theirry, ambaye amesisitiza kukitengeneza kikosi chake ambacho kina maingizo ya wachezaji wapya waliosajiliwa mwezi mmoja uliopita.

Kichuya aliyeingia kipindi cha pili kwenye mchezo dhidi ya Tanzania Prisons uliochezwa mjini Sumbawanga mkoani Rukwa akichukua nafasi ya Abeid Athuman, amesema kikosi chao kinaundwa na wachezaji wengi wageni, hivyo siyo kazi rahisi kwa kutengeneza muunganiko katika muda mfupi.

“Mashabiki watakiwa kuwa na subra katika michezo hii ya awali na kumuacha kocha afanye kazi ya kutengeneza kikosi cha ushindani kwani bado tuna michezo mingi pia tuna michezo ya kimataifa,” amesema Kichuya.

Amesema Ligi Kuu imekuwa na ushindani mkubwa kwani kila timu inapania kuibuka na ushindi, hivyo kikosi kikiwa na makosa wapinzani wanatumia fursa hiyo kupata ushindi.

Kichuya amesema bado anaamini kikosi chao kina wachezaji wengi wazuri lakini kocha bado anatafuta kikosi cha kwanza, ndio maana hata yeye kwenye baadhi ya michezo amekuwa anaanzia benchi.

Namungo FC mwishoni mwa juma hili watacheza dhidi ya Mbeya City katika mchezo wa mzunguuko wanne wa Ligi kuu, Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Amuua mwanae akitaka kujua jinsia
Mali yateua serikali mpya