Mbunge wa Jimbo la Mtama Nape Nnauye, amehoji kwamba ni lini sasa serikali itaweka utaratibu kwa wanafunzi wa kidato cha Tano na Sita kuacha kulipa Ada ili nao wawe kama wale wa chekechea hadi kidato cha Nne wanaopata elimu bila malipo.
Amesema hayo Bungeni Jijini Dodoma, wakati wa kipindi cha maswali na majibu, swali lililoelekezwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na lilijibiwa na Naibu Waziri Omary Kipanga.
“Pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na serikali ya kugharamia elimu kutoka chekechea hadi kidato cha nne na utaratibu wa kutoa mikopo kwa Elimu ya Juu bado vijana wa Kidato cha 5 na cha 6 kuna tatizo la kugharamia elimu, ni lini sasa serikali itaweka utaratibu ili kuwahusisha vijana hawa kuwa kwenye utaratibu wa elimu bila malipo?” amema Nape
“Ni kweli vijana wetu wa kidato cha 5 na 6 wanatakiwa kulipa Ada ambayo ni Tsh 70,000 kwa Bweni na 35,000 kwa wale wa kutwa, Ada hii tunaiona ni affordable na Watanzania wengi wanaweza kuilipa, wacha tulibebe tuliangalie kwa kina ili tuone katika kipindi kijacho kama tunaweza kuiondoa Ada hii” amejibu Naibu Waziri Omary Kipanga